Public Health Education
SIKU YA KICHAA CHA MBWA DUNIANI: September 28.
Na Dr. Taphinez Machibya.
Kichaa cha Mbwa ni ugonjwa hatari unaosababishwa na Virusi aina ya Lyssa. Ugonjwa huwapata wanyama na binadamu huupata pia kwa kuumwa na wanyama Kama Mbwa, Mbwa mwitu, paka, Fisi, popo na wengineo wa jamii hiyo mwenye kichaa cha Mbwa.
Binadamu pia anaweza kuambukizwa kwa kugusa au kuingiwa na mate ya mnyama aliyeathirika, kupitia jeraha, mchubuko, jicho, pua au mdomo. Virusi hawa wanapoingia mwilini kwa mtu huenda hadi kwenye ubongo kupitia mzunguko wa damu ambapo huanza kuleta mashambulizi katika mishipa ya mfumo wa fahamu mpaka mtu kufikia hali ya kichaa cha Mbwa.
CHANJO KWA WANYAMA.
Kumekuwa na utamaduni wa baadhi ya watu kufuga Mbwa kama utamaduni au mazoea au kujifurahisha tu bila lengo mahsusi hasa. Wapo wanaofuga wanyama hawa kwa kusudi la ulinzi na usalama wa nyumba na mali zao. Lakini kuna changamoto hasa katika malezi na matunzo ya wanyama hawa mtaani au katika nyumba nyingi maana wanahitaji huduma za afya pia kama binadamu na hasa chanjo ya wanyama pamoja na magonjwa mengineyo ya wanyama.
Wito wangu leo ni kuhusu kuwakinga Wanyama wetu hawa hasa Mbwa kwa kuwapatia chanjo kila mwaka au kulingana na ushauri wa mtaalamu wa mifugo. Ikiwa huoni sababu ya kumchanja au kumhudumia ni afadhali usimfuge kabisa mnyama huyu Mbwa.
Ninaongea hivi kwa uchungu na masiktiko pia kwa sababu hata katika kituo changu cha kazi, tumekuwa tukipokea wagonjwa tofauti wenye historia ya kung’atwa na Mbwa kisha wanakuja na dalili za kichaa cha mbwa na wengi wameishia kupoteza maisha. Wengine ni ndugu zetu kabisa. Hata mimi binafsi nina rafiki yangu wa karibu sana amempoteza mpwa wake mwezi huu huu wa September 2020, kwa mtoto kuumwa na Mbwa na baadaye kuonesha dalili hizi za Kichaa cha Mbwa hadi kifo. Inasikitisha sana.
JINSI YA KUHUDUMIA JERAHA LILILOTOKANA NA KUNG’ATWA NA MNYAMA.
Endapo mtu atang’atwa na Mbwa au mnyama mwingine yoyote, aoshe sehemu ya jeraha kwa maji mengi yanayotiririka na sabuni kwa angalau dakika 15. Pia Iodine yaweza kutumika. Kidonda kisifungwe na mhanga apelekwe hospitali au kituo cha Afya kupatiwa chanjo ili kuzuia madhara dhidi ya kichaa cha Mbwa.
DALILI ZA KICHAA CHA MBWA.
Inamchukua mtu siku kadhaa mpaka hata miaka kadhaa kuanza kuonesha dalili za kichaa cha Mbwa. Inategemea pia sehemu ya jeraha la kung’atwa ilipotokea. Kwa mfano aliyeng’atwa sehemu ya kichwa au shingo ataonesha Dalili mapema zaidi kuliko aliyeng’atwa mguuni. Lakini muda wa wastani wa dalili kuanza kuonekana ni mwezi 1 hadi 3. Kasi ya kusafiri kwa virusi wa Kichaa cha Mbwa mwilini kufuata mkondo wa neva za fahamu (Axons) hadi afikie katika ugwemgongo (Spinal ganglion) ni mm 12-24 kwa siku. Na akishafika katika uti wa mgongo kuelekea ubongoni huenda kwa kasi zaidi ya mm 200 - 400 kwa siku.
Dalili hizo ni kama viel:
1. Homa
2. Maumivu ya kichwa na viungo mbalimbali
3. Muwasho sehemu ya jeraha
4. Kuogopa mwanga
5. Kuogopa kunywa maji
6. Kukosa hamu ya kula
7. Kukosa usingizi
8. Kichefuchefu na au kutapika
9. Kuanza kubweka kama mbwa
10. Kutiririkwa mate ovyo mdomoni (akiwa na historia ya kung’atwa na dalili zingine)
11. Kuchanganyikiwa, kuvunja au kupiga vitu ovyo
12. Kuweweseka au kushtuka mara kwa mara
13. Kupoteza fahamu
14. Kupooza, kudhoofu na hatimaye kupoteza maisha.
TAHADHARI:
1. Usimsogelee wala kumchokoza Mbwa au mnyama yeyote mwenye dalili za kichaa cha mbwa.
2. Waelimishe watoto kuepuka kuchokoza au kupiga mbwa, Pia kutoa taarifa kwa wazazi endapo watapata tukio la kukwaruzwa, kungatwa au kulambwa sehemu yenye jeraha na mbwa.
3. Toa taarifa kwa mtaalamu wa mifugo au uongozi wa serikali za mitaa, kijiji au kata ili mnyama husika adhibitiwe.
4. Zuia uzururaji wa mbwa kwa kumfungia katika banda , uzio au kumfunga kamba kuanzia saa 12 alfajiri na kumfungulia saa 4 usiku.
5. Epuka kugusa mizoga ya wanyama waliokufa au wanaoonesha dalili za kuumwa kama Mbwa, paka, popo n.k
6. Kwa watumishi wa afya pia tunapohudumia mgonjwa wa Kichaa cha Mbwa chukua tahadhari zote na vaa vifaa kinga vyote vinavyohitajika kukulinda.
JINSI YA KUMHUDUMIA MGONJWA WA KICHAA CHA MBWA.
1. Ikiwa mtu kang’atwa na mnyama asafishwe jeraha , angalia kama kuna meno ya mnyama yaliyobaki, yatolewe na kidonda au jeraha liachwe wazi
2. Mpeleke hospitali haraka iwezekanavyo
3. Ikiwa tayari ameonesha dalili za kichaa cha Mbwa Chukua tahadhari ya kutong’atwa na mgonjwa au kudondokewa na mate, damu au majimaji yanayotoka kwa mgonjwa wa kichaa cha Mbwa.
4. Mweke katika sehemu tulivu isiyo kuwa na kelele na mwanga mkali
5. Usimlazimishe kunywa majimaji au kula maana tayari ana madhara katika mfumo wa fahamu
6. Afikapo hospitali atahudumiwa kulingana na uhitaji wake.
ANGALIZO: Kumekuwa na udanganyifu kwa baadhi ya watoto huduma za afya hasa kwa wagonjwa wasio na ufahamu kuhusu tiba na chanjo ya kichaa cha Mbwa, hii imepelekea watu kupewa dawa zisizo sahihi na kuleta madhara kwa wagonjwa hawa baadaye na hatimaye kifo.
OMBI: Niwaombe wataalamu wenzangu wa Afya kuzingatia Maadili ya kazi kwa kutoa kitu kilicho sahihi kwa Mgonjwa au mtu aliyeng’atwa. Pia tusiwauzie watu dawa au chanjo (Anti rabies Vaccine/ Immunoglobulins) zisizo halisi au za kweli. Tatizo la Kichaa cha Mbwa ni halisi na linaua sana tu.
Niwaombe pia wananchi kufika vituo vya afya kupata chanjo ambayo haiuzwi, isipokuwa Immunoglobulins ambayo pia ukihitajika kuchangia malipo, fika dirisha la Malipo la hospitali, lipia huduma na pewa stakabadhi ya malipo halali na siyo kulipia pembeni kwa mtu, utadanganywa na utalia baadaye. Mbaya sana unaweza usipate tiba sahihi. Vinginevyo unaweza kudanganywa kupewa kitu tofauti na chanjo ya kichaa cha Mbwa na ukaja kupata madhara baadaye kwako, mtoto, ndugu au jamaa yako wa karibu. Wengi wanaishia kupoteza maisha. Fuata utaratibu sahihi. Pata tiba sahihi.
Niwaombe pia wataalamu wa Afya ya Mifugo kujitokeza, kuwafikia wananchi, na kuwaelekeza huduma za afya kama tiba na chanjo ya wanyama kama Mbwa, paka inakopatikana kwa urahisi.
MWISHO: Ni vizuri ukipata chanjo mara tu baada ya kung’atwa Na Mnyama kabla hujaonesha dalili zozote kwani ugonjwa huu hauna tiba.
read more