Hospitali ya Rufaa Mkoa wa Katavi
(Mpanda Hospitali)

WAZIRI MHAGAMA AGAWA MASHINE 185 ZA UCHUNGUZI WA KIFUA KIKUU NCHI NZIMA

Posted on: January 6th, 2025

Katika jitihada za kudhibiti na kutokomeza ugonjwa wa Kifua Kikuu nchini Tanzania ifikapo 2030, Serikali imegawa mashine mpya 185 zenye thamani ya Shilingi Bilioni 7 kwa ajili ya uchunguzi na ugunduzi wa vimelea vya ugonjwa huo nchini.

Kauli hiyo imetolewa na Waziri wa Afya Mhe. Jenista Mhagama, Jana Januari 6, 2025 kwenye hafla ya ugawaji wa mashine hizo iliyofanyika katika Kituo cha Afya Chamwino, Dodoma iliyoenda sambamba na uzinduzi wa Mpango harakishi wa kuibua wagonjwa wa Kifua Kikuu katika Halmashauri 76 za mikoa tisa (9).

Waziri Mhagama amesema Tanzania inafanya vizuri kwenye mapambano dhidi ya ugonjwa wa Kifua Kikuu ambapo kwa sasa ni nchi ya Sita kati ya nchi zote zinazofanya vizuri lakini bado juhudi zinaendelea ili kufanya vizuri zaidi kwa kuwa bado tupo ndani ya nchi 30 zenye maambukizi makubwa.